Thursday, September 18, 2014


Wakala waChuo Cha Taifa Cha Utalii waendelea kukua
·      Zamani ilijulikana kama Chuo cha Hoteli na Utalii Forodhani


Na Beatrice Discoryce
Unapopita katika Makutano ya Barabara ya Samorana Mtaa wa Shaban Robert, Jijini Dar es Salaam, jirani na yalipo Makao Makuu ya Wizara ya Afya na Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kuna jengo zuri jeupe, unaweza ukadhani kwamba hiyo ni hoteli ya kifahari, la hasha, kumbe hapo ni Makao Makuu ya Wakala wa Chuo Cha Taifa cha Utalii na Kampasi ya Bustani,  sehemu ya wahitimu wanataaluma ambao ni wachangiaji wa pato la Taifakwa wastani wa shilingi trilioni mbili na ushee kwa mwaka.

Hapo ni mahali pekee ambapo kijana wa Kitanzania anapohitimu masomo yake anatembea kifua mbele pasi na shaka ya kupata ajira, kwani wahitimu wa chuo hicho ni lulu serikalini  na kwa wawekezaji katika sekta ya Utalii.
Lakini wengine hujiajiri na kuyanawirisha maisha yao, wengi wao hivi sasa wanamiliki mighahawa, mahoteli na makampuni ya kitalii kona mbalimbali za nchi yetu.

Tanzania kama nchi nyingine Duniani kote, kuna changamoto ya ajira kwa vijana, lakini ni nadra sana kumpata kijana aliyehitimu katika taasisi hiyo akirandaranda mtaani kutafuta ajira kwani kwani chuo kinazalisha vijana ambao wameiva kitaaluma, ki-nadharia na ki- vitendo. Kizuri zaidi ni kuwa chuo hicho mali ya Umma, heshima yake haijashuka tangu kianzishwe, miaka ya nyuma kilijulikana kama Chuo cha Mafunzo  ya Hoteli na Utalii Forodhani  na kilikuwa eneo la barabara ya Kivukoni mahali ilipo Mahakama ya Rufaa.

Ili kuhakikisha kwamba wahitimu wanakuwa bora, mafunzo ya vitendo huchukua asilimia 60 wakati nadharia huchukua asilimia 40 iliyobaki, wakitengewa pia muda wa kutosha wa kufanya mazoezi kazini.

Uongozi wa chuo hicho unasema mwaka jana pekee takribani vijana 173 walihitimu katika Chuo hicho, asilimia kubwa wameajiriwa wengine wamejiari na wengine wanaendelea  na masomo ya juu  vyuo mbalimbali.
“Tumewafuatilia Wahitimu wetu na kubaini kuwa asilimia kubwa wamepata ajira katika sehemu mbalimbali, wengine serikalini lakini wengi zaidi sekta binafsi ambako biashara ya hoteli na Utalii kwa ujumla imepamba moto, vijana wetu wamebobea katika fani za utunzaji na uaandaji wa vyumba,Mapishi,Uokaji,Uhudumiaji wageni,Uongozaji watalii na Mapokezi ya wageni hotelini na Utalii,”

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo hicho Rosada Msoma, ambacho pia ni Wakala wa Serikali tangu mwaka 2003 anafafanua kuwa wahitimu wetu wao wako kwenye sekta kiongozi katika uchumi, sekta inayoshika nafasi ya tatu kwa kuliingizia Taifa pato kwa mwaka, yaani sekta ya Utalii.

Wachumi wanasema mapato katika sekta hiyo kwa mwaka 2013 yalikuwa ni Sh trilioni 2.96 baada ya kupokea watalii 1,095,884 yakiongezeka kutoka Sh. trilioni 2.69 za mwaka 2012 zilizotokana na watalii 1,077,058 waliongia nchini.
“Kwa hiyo ni jinsi gani unaweza kuona Chuo chetu kilivyo muhimu katika maendeleo ya sekta hiyo hasa kwa kuzalisha vijana ambao wanaweza kazi zao kwa ufanisi mkubwa kutokana na kusomeshwa vizuri ,”anasema.

Anabainisha kuwa ubora wa mafunzo unatokana na ubora wa Waalimu ambao nao pia wamesomeshwa vizuri na serikali.

“Tuna vifaa vya kisasa kuliko chuo chochote cha aina ya kwetu hapa Afrika Mashariki, tuko vizuri, ndiyo maana hata vijana wanapotoka hapa hawaangaiki kutafuta kazi,waajiri wenyewe wanawakubali.

Anafafanua kuwa Chuo chake kimesajiliwa na NACTE kutoa elimu kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada.

“Tunatoa mafunzo bora kulingana na mahitaji ya soko,mafunzo ambayo pia yanamuwezesha muhitimu si kuajiriwa tu na hata kujiajiri, wapo waliojiajiri na ambao kwa kweli wanafanya vizuri sana kwenye biashara zao, na wengine ni wafanyabiashara wakubwa katika sekta ya Utalii lakini wamepitia hapa hapa,” anasema.

Katika kusaka elimu wapo wenye kiu ya kuendelea na mafunzo ya juu zaidi anasema baadhi yao hivi sasa wako katika ngazi mbalimbali za viwango vya elimu kwa maana wengine wanasomea Shahada ya kwanza.”

“Wako waliopita hapa kwa sasa ni wasomi wazuri na wanafanya shughuli zao mbalimbali, kwa kuwa hiki ni Chuo cha serikali, ni rahisi mhitimu kujiendeleza zaidi kielimu,kwani ni chuo kinachotambulika,hivyo kuwa rahisi kwa wahitimu wetu kuendlea na elimu ya ngazi ya Chuo Kikuu.

Anasema Chuo kina kampasi tatu ambazo zinatoa mafunzo katika ngazi ya Astashahadana Stashahada, anazitaja kampasi hizo kuwa ni Bustani ambayo pia ni Makao Makuu ya Chuo hicho ambayo inafundisha kozi Ukarimu (Hospitality) kampasi hii ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 360.

Kampasi nyingine ni ya Temeke, yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150, na inafundisha kozi ya Utalii wakati ile ya Arusha inachukua wanafunzi 120 na inafundisha kozi ya Ukarimu (Hospitality). “Jumla Wakala una uwezo wa kuchukua vijana wa mia sita thelathini (630) hivi,” anasema.

Bi.Msoma anafafanua kuwa kozi za Ukarimu ngazi ya Astashahada huchukua miaka miwili ambayo hujumuisha masomo ya Mapishi (Food Production),Utoaji huduma ya vyakula na Vinywaji, (Food and Beverage Services),Utunzaji Vyumba (Accomodation Operations), Uokaji (Pastry and Bakery) na Mapokezi ya Wageni Hotelini ( Front Office Operations).

Kwa ngazi ya Stashahada anasema inajumuisha masomo ya Mapishi(Culinary Arts),Utoaji huduma ya Vyakula na Vinywaji, Utunzaji na Ugawaji wa Vyumba (Rooms Division).

Kozi za Utalii ngazi ya Astashahada anasema  inajumuishamasomo ya Uongozaji Watalii (Tour Guiding Operations) mwaka mmoja, Usafiri na Utalii (Travel and Tourism) miaka miwili.Ngazi ya Stashahada inajumuisha Usafari naUtalii (Travel and Tourisim) miaka miwili pia.

Bi.Msoma anasema kuwa ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanamudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi,chuo pia hufundisha masomo ya Kiingereza na Kifaransa, TEHAMA (Teknolojia ya Habari  na Mawasiliano), Ujasiriamali,Rasilimali watu na Huduma kwa mteja.

“Pia Wakala hutoa kozi za muda mfupi kulingana na mahitaji ya wateja katika fani za Utalii na Ukarimu,”
Anasema Chuo pia hutoa huduma za Utafiti na Ushauri katika Nyanja za Utalii na Ukarimu.

Anabainisha kwamba ili kutoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo, kampasi zote tatu, Bustani,Temeke na Arusha hutoa huduma ya vyakula na kumbi za mikutano ambapo huduma hizi huchangia pato la ndani la Wakala.
Anayataja mafanikio ya Chuo hicho kuwa ni,kupanuka kwa Chuo, kwa maana ya kujitanua na kuwa na majengo ya kutosha kufanyia shughuli zake za ufundishaji kwa nadharia na vitendo.

Chuo kuwa Wakala wa serikali mwaka 2003,Chuo kuwa na majengo mazuri na vifaa vya kisasa vyenye technolojia ya hali ya juu katika kampasi kampasi ya Bustani.

Mengine ni kupanuka kwa Chuo kutoka Kampasi moja yenye uwezo wa wanafunzi 150 kufikia wanafunzi 630 kwa kampasi tatu, ambapo imeongeza uwezo wa kudahili kufikia wanafunzi 315 kwa mwaka.

Mengine ni kuongezeka kwa programu za mafunzo ya usafiri na Utalii kwa ngazi ya cheti.
Kuanzishwa kwa Programme ya Apprenticeship kwa kushirikiana na Sekta binafsi pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Programme inatoa  nafasi kwa kijana kufanya kazi na kusoma, pia anakuwa na uhakika wa kupata ajiri mara anapofanikiwa kusoma.

Kuanzishwa na kuimarishwa kwa ofisi ya Mrajisi na mitihani chuoni, ambapo kumepelekea utoaji wa mafunzo katika viwango vya Baraza la elimu ya Ufundi(NACTE).

Programu za mafunzo yatolewayo katika kampasi zote tatu zinatambuliwa na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Ukarabati wa hostel za kulala wanafunzi na kuongeza uwezo wake toka wanafunzi 60 hadi wanafunzi 120.

Anasema kwamba mwaka 2007 walikuwa na Kampasi moja tu iliyoko Temeke, baadaye wakafungua kampasi Arusha na kisha mwaka 2011 wakafungua kampasi ya Bustani. “Ni mafanikio makubwa sana kupanua huduma zetu,”

“Mafanikio mengine ni ujenzi wa jengo letu la Makao Makuu chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD),” Anasema kupatikana kwa Majengo ya Arusha kutoka kwa wafadhili wa Hans Seidel Foundationpia ni mafakio yalichochea ukuaji wa kasi wa Chuo chetu,”.

Kuhusu historia ya Wakala, Wakala umerithi Chuo cha Mafunzo ya Hotel naUtalii (HTTI), maarufu kama Chuo cha Hoteli na Utalii Forodhani, iliyoanzishwa mwaka 1969 chini kampuni ya hoteli ya Kiingereza ya Hallmark Hotels, lengo lake lilikuwa ni kutoa mafunzo ya  msingi kwa watumishi mbalimbali wa Hoteli.

Taasisi hiyo ilikabidhiwa mara ya kwanza serikalini mwaka 1977 kupitia Wizara ya Maliasili naUtalii, kutokana na mahitaji ya kuboresha huduma na kukua kwa sekta ya Utalii nchini.

Anasema Dira ya Wakala ni kuwa kituo bora Afrika katika kutoa mafunzo bora katika fani za Ukarimu na Utalii, na Dhima ya Wakala ni kutoa mafunzo bora utafiti na huduma ya ushauri katika sekta ya Ukarimu na Utalii kwa kutumia watumishi wenye weledi na vifaa vya kisasa ili kufikia matarajio ya wateja.

Wakala unatekeleza majukumu yake kwakufuata Malengo ya Mpango Mkakati wa Wakala wa mwaka 2014/15 -2016/17 unaotekelezwa kwa sasa, Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999,Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2010-2015,Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2011-2016, na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025

Anasema Chuo ni Wakala pekee wa Serikali unaotoa mafunzo katika fani za Ukarimu na Utalii. Hivyo wanatoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne, kidato cha sita na wale wanaomaliza miaka mitatu VETA katika fani ya Ukarimu na Utalii wachangamke fursa ya kujiunga na chuo chao.
Mwisho


Tuesday, March 1, 2011

Saturday, February 26, 2011

Saturday, February 19, 2011

Sunday, February 13, 2011